Friday, 1 September 2017

BODI YA MIKOPO(HESLB): MUDA WA KUTUMA MAOMBI WAONGEZWA HUKU 15,473 PEKEE NDIO WALIOKAMILISHA TARATIBU ZA KUTUMA MAOMBI

Image result for HESLB

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeongeza muda wa siku saba kuanzia Septemba 4, 2017 hadi 11, mwaka huu ili waombaji wenye sifa wawasilishe maombi yao kabla ya kufungwa kwa dirisha la maombi.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu mchakato wa uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2017/18 na kwamba HESLB imetenga jumla ya Sh bilioni 427 kwa mikopo yote. Kwa mujibu wa Badru, jumla ya wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza wa masomo wa 2017/18, wanatarajiwa kupata mikopo ya elimu ya juu huku wanafunzi 93,292 wakiwa wanaendelea kupokea mikopo hiyo kwa ajili ya kukamilisha masomo yao.
Badru alisema hadi kufikia juzi, jumla ya waombaji wa mikopo kwa njia ya mtandao walikuwa 49,282, kati yao waombaji 15,473 wakiwa wamekamilisha maombi yao kwa njia ya mtandao kwa kufuata taratibu zote za uombaji zilizotolewa na Bodi. Alisema kwa takwimu za maombi hayo, wapo waombaji 33,809 ambao wapo katika hatua mbalimbali za kuambatanisha nyaraka zao za maombi na kuwataka wale ambao hawajakamilisha kuwasilisha maombi yao ya mikopo kama ilivyoelekezwa.
Alisema waombaji wa mkopo wanatakiwa kuambatanisha nyaraka zao kwenye mfumo wa mtandao wa maombi hayo (OLAMS) kukiwa na nyaraka zilizosainiwa na viongozi wa serikali za mitaa na makamishna a viapo au Hakimu na kuziweka katika mtandao huo. Badru aliwataka wale wanaotarajia kuomba, kutumia muda uliosalia kukamilisha maombi yao, na kuyawasilisha kwa mujibu wa maelekezo, huku wakitakiwa kusoma kwa makini maelekezo na kufuata hatua zote za kukamilisha maombi ya mikopo.
Alisema bodi ilifungua dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2017/18 kwa mwezi mmoja kuanzia Agosti 6, 2017 ili kuwawezesha waombaji wenye sifa kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mtandao (OLAMS).
Alisema mchakato wa kuomba na kupanga mikopo unaongozwa na sheria iliyoanzisha Bodi ya Mikopo na miongozo inayoainisha sifa, utaratibu na hatua muhimu kwa waombaji wa mikopo. Badru alizitaja hatua muhimu kwa waombaji wa mikopo kuwa ni pamoja na kila muombaji kutakiwa kuwasilisha nyaraka za maombi ikiwemo fomu ya maombi iliyosainiwa na Kamishna wa viapo au wakili na Hakimu, nakala za vyeti vya taaluma zilizothibitishwa na kugongwa muhuri na kamishna wa viapo, wakili au Hakimu.

No comments:

Post a Comment