Saturday, 13 May 2017

PIGO:MWAMBUNGU,SOZIGWA HATUNAO TENA

Image result for MWAMBUNGU
TAIFA limepata pigo la kuondokewa na watumishi wa Serikali wa muda mrefu, mwanahabari nguli aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kwanza wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, Paul Sozigwa na aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu.
Wawili hao walifikwa na mauti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) walikokuwa wamelazwa kwa matibabu. Sozigwa ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Kwanza wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD, sasa TBC baada ya kuwa Shirika la Utangazaji Tanzania), alifikwa na mauti jana saa nane usiku wa kuamkia jana kutokana na matatizo ya moyo , wakati Mwambungu pia aliaga dunia jana asubuhi kutokana na maradhi ya figo.
Msemaji wa JKCI, Anna Nkinda alithibitisha kutokea kwa vifo vya Mzee (84) aliyekuwa amelazwa tangu Aprili 25, mwaka huu akitokea Wodi ya Mwaisela ya Hospitali ya taifa Muhimbili (MNH) na Mwambungu (62) ambaye alifikishwa hospitalini hapo Mei 10 mwaka huu saa nane mchana.
Mtoto wa kwanza wa marehemu, Hamidu Mwambungu alisema baba yake alikuwa akisumbuliwa na tatizo la figo kwa zaidi ya mwaka mmoja na ni ugonjwa ambao umemsababishia mauti hayo.
Alisema familia inaendelea kupanga taratibu za maziko. “Hatujajua mazishi yatafanyika lini na wapi bado wanafamilia tunakutana kupanga lakini nadhani tunaweza kuzika mwishoni mwa wiki hii,” alisema Hamidu. Hamidu alisema msiba huo uko nyumbani kwa marehemu Tabata Kimanga, Dar es Salaam.
Mzee Sozigwa “Mzee Sozigwa alikuwa akisumbuliwa magonjwa mengine pia, aliletwa hapa akiwa na tatizo la moyo, akatibiwa hapa akawa amepona lakini alibaki hapa wakati akiendelea na matibabu ya yale magonjwa mengine mpaka leo (jana) alipofariki,” alisema Nkinda.
Mtoto wa marehemu, Mchungaji wa Kanisa la KKKT, Moses Sozigwa alisema baba yake alikuwa akisumbuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo, matatizo ya tumbo, na pia shida mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupoteza kumbukumbu inayotokana na kuwa na umri mkubwa.
Aidha, alisema familia inaendelea kupanga mazishi ya baba yao na kwamba msiba huo uko nyumbani kwake Mtoni Mtongani, Temeke kwenye Kanisa la KKKT ambako ni maarufu kama maskani ya Kwaya ya Lulu.
Mbali ya kuwa Mkurugenzi wa RTD na baadaye mwaka 1967 kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais, Sozigwa alikuwa kada mzuri wa chama tawala, CCM alikokuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Pwani, lakini pia akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho. Sozigwa atakumbukwa kutokana na weledi na uadilifu wake katika kutimiza majukumu yake.
CCM kimetoa salamu za rambirambi kwa msiba huo wa Sozigwa ambapo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole amesema kuwa chama kimepokea kwa masikitiko taarifa za msiba huo. “Mzee Sonzigwa alihudumia na kutoa huduma kwa utumishi uliotukuka ndani ya chama na pia serikali kabla na baada ya uhuru na pia alihudumia kama katibu wa kwanza wa Rais Mwalimu Nyerere,” alisema Polepole.
Alisema chama hicho kitamkumbuka na kumuenzi na jambo ambalo alishughulika nalo ni pamoja na kushughulikia misingi na maadili na miiko ya uongozi ndani ya CCM. Naye Naibu Katibu Mkuu CCM (Bara),Rodrick Mpogolo, amemtaja Mwambungu kuwa alikuwa kiongozi mwadilifu katika utendaji wake wa kazi ndani ya CCM alipokuwa Mkuu wa Utawala Makao Makuu (Ofisi Ndogo) Lumumba, Dar es Salaam na hata alipoteuliwa kuwa mtumishi wa Serikali.
“Tumempoteza kiongozi mahiri na shupavu … watu wanakumbukwa kwa yale mazuri unayofanya hapa duniani na Mwambungu atakumbukwa kwa mema aliyoyetenda wakati wa uhai wake,” alisema Mpogolo akiwa mjini hapa.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) mkoa wa Morogoro, Christine Ishengoma, alisema alimfahamu Mwambungu wakati yeye (Dk Ishengoma) alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani mwaka 2006 na aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
“Nimeshistushwa na kifo chake …ninaweza kusema kuwa Mwambungu ndiye aliyenipokea wakati nikiwa mkuu wa mkoa wa Pwani na yeye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha na makao makuu ya mkoa ni Kibaha,” alisema Dk Ishengoma.
Pamoja na hayo alisema kuwa, mara baada ya Mwambungu kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa na kupangiwa mkoa wa Ruvuma, Dk Ishengoma alisema alimpokea na kukabidhi mkoa huo wakati yeye akihamishiwa mkoa wa Iringa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe, alimtaja Mwambungu kuwa licha ya kumfahamu kupitia vyombo vya habari, alifahamiana yake wakati walipoteuliwa kuwa wakuu wa mikoa.
“Mwambungu alikuwa mcheshi, alikuwa karibu na wananchi na pia ni mpenda utani ni hazina kuu imepotea, lakini ni mapenzi ya Mungu,” alisema. Baadhi ya viongozi wa CCM, wakiongozwa na Mwenyekiti wao mkoa wa Morogoro, Innocent Kalogeries na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro mjini kichama, Fikiri Juma kwa nyakati tofauti waliwajulisha wajumbe walioshiriki kikao hicho juu ya kutokea kwa msiba huo.

No comments:

Post a Comment