Wajawazito wanapenda kuongea na mimba zao, na baadhi ya ndege wazazi pia wanapenda kuimba wimbo maalum mbele ya mayai wanayoangua. Kwa nini wanafanya hivi?
Ripoti iliyotolewa kwenye gazeti la Sayansi imeeleza tabia hii ya kipekee ya ndege aina ya shorewanda milia. Watafiti walifikiri tabia hii huenda inahusiana na hali ya hewa, kwa sababu ndege wazazi wanapenda zaidi kuimba wimbo maalum hasa wakati hali ya hewa inapokuwa joto sana na katika kipindi cha mwisho cha kuangua mayai.
Bibi Mylene Mariette na Katherine Buchanan kutoka Chuo Kikuu cha Deakin cha Australia walirekodi wimbo maalum wa ndege wazazi, na kuyafanya baadhi ya mayai kwenye mashine ya kuangua mayai kusikiliza wimbo huo, na mayai mengine kusikiliza sauti ya kawaida ya ndege wakubwa.
Baada ya ndege wachanga kuzaliwa, watafiti hao waligundua kuwa ndege waliozaliwa kutoka kwenye mayai yaliyosikiliza wimbo maalum wana miili midogo zaidi kuliko wale waliosikiliza sauti ya kawaida. Miili midogo inamaanisha kuwa wanaweza kupunguza joto la miili vizuri zaidi na kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kunusurika katika mazingira yenye joto kali.
Watafiti wamesema katika kipindi cha mwisho cha kuangua mayai, mfumo wa kurekebisha joto la mwili unaanza kukua, ndege wazazi wanarekebisha kasi ya ukuaji wa ndege wachanga kwa wimbo wao. Hii ni njia ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo haijagunduliwa kabla ya hapo.
No comments:
Post a Comment