WOSIA ulioachwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aboud Jumbe Mwinyi umezidisha simanzi katika kifo chake kilichotokea Dar es Salaam jana.
Wakati wa uhai wake, Jumbe (96) aliagiza maziko yake kuwa ya kawaida kwa mujibu wa misingi ya dini ya Kiislamu, ingawa familia yake imesema hatua hiyo haiwazuii viongozi wa serikali kuhudhuria shughuli nzima za mazishi yake.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa Jumbe, Mjimwema Kigamboni, Dar es Salaam jana, msemaji wa familia, mtoto wa marehemu, Mustafa Aboud Jumbe pamoja na kueleza kuwa marehemu atazikwa katika makaburi ya Migombani, mjini Unguja Zanzibar leo, alisema sharti lililowekwa na kiongozi huyo la maziko yake kuwa ya kawaida na ya misingi ya dini, litazingatiwa kama alivyoagiza wakati wa uhai wake.
Mustafa, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi ya Zanzibar, alikuwa akizungumza juu ya kutokea kwa kifo hicho, ambacho alisema kimesababishwa na maradhi ya utu uzima.
“Marehemu atazikwa kwa maziko ya kawaida ya Kiislamu kwa mujibu wa maagizo yake aliyoyaacha, na sisi tunayaheshimu hayo maagizo. “Lakini haizuii viongozi wa Serikali kushiriki shughuli hii. Unajua mzee alikuwa mtu wa dini sana, kwa hiyo mwenyewe alituusia hivyo atakapokufa basi azikwe maziko ya Kiislamu kwa mujibu wa dini yetu,” alisema Mustafa ambaye ni mtoto wa tano wa Jumbe.
Alisema mwili wake utasafirishwa leo asubuhi kuelekea Zanzibar kabla ya kupelekwa katika Msikiti wa Mwembeshauri mjini Unguja saa sita adhuhuri kwa ajili ya kuuswalia na kisha kuzikwa katika makaburi ya Migombani mjini humo.
Rais Magufuli atuma salamu Katika tukio jingine, Rais John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein kutokana na kifo hicho.
Katika salamu zake jana, Rais Magufuli alisema “Nimeshitushwa sana na kifo cha Mzee wetu Mheshimiwa Aboud Jumbe, kwa hakika Tanzania imepoteza mtu muhimu ambaye katika kipindi cha uongozi wake, alitoa mchango mkubwa wa kuipigania na kuijenga Tanzania tunayoiona leo.”
Jumbe alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Mwaka 1972 hadi 1984.
Rais Magufuli alisema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alijitoa kupigania uhuru, umoja, haki na maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kipindi kigumu ambacho Taifa lilikipitia.
“Kupitia kwako Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein napenda kuwapa pole familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote, wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa ujumla kwa kufikwa na msiba huu mkubwa,” alisema Rais Magufuli Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, January Makamba akizungumza na gazeti hili jana alisema wamepokea taarifa ya msiba huo kwa masikitiko na tayari maandalizi ya mazishi ya kiongozi huyo yanafanyika baina ya serikali na familia yake.
“Tumepokea taarifa za kifo kwa masikitiko makubwa kwa kuondokewa na kiongozi wetu, kichama na serikali, tayari Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameshaenda Zanzibar kwa ajili ya maandalizi hayo. “Mwili wa marehemu utasafirishwa kesho (leo) kwenda Zanzibar na baadaye maziko yatafanyika saa saba mchana na yataongozwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali.”
Jumbe atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akichukua nafasi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Abeid Amaan Karume aliyefariki mwaka 1972.
Enzi za uhai wake akiwa Rais wa Serikali ya mapinduzi Zanzibar alishirikiana na Rais wa wakati huo wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha TANU, Julius Nyerere kuanzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuunganisha vyama vya TANU na ASP na kuunda chama kimoja.
Kwa upande wake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza kusikitishwa na kifo hicho cha Jumbe. Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud mjini Zanzibar jana ilisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikitishwa na kifo hicho.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikitishwa na kifo cha Alhaji Aboud Jumbe ambaye alikuwa Rais wa Zanzibar kwa muda wa miaka 13 huku mchango wake mkubwa katika kukuza na kuimarisha demokrasia ukibakia kielelezo kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa za kutoka kwa familia ya Jumbe, maziko yake yanatarajiwa kufanyika leo mchana nyumbani kwake Migombani nje kidogo ya mji wa Zanzibar, eneo ambalo watoto wake watatu wamezikwa hapo.
Historia yake kisiasa
Jumbe alishika madaraka ya kuongoza Zanzibar katika mwaka 1972 baada ya kuuawa kwa Abeid Amaan Karume ambapo Baraza la Mapinduzi kwa kauli moja lilimchagua kushika wadhifa huo wa Rais wa Zanzibar.
Kutokana na kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar katika mwaka 1984, Jumbe alilazimika kujiuzulu pamoja na viongozi wengine akiwemo Waziri Kiongozi Ramadhan Haji Faki na hivyo kupoteza nyadhifa zote, ikiwemo Makamu wa Rais wa Muungano na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Jumbe atakumbukwa kwa mambo mengi akiwa ni mmoja ya viongozi walioshirikiana na Mwalimu Nyerere kuzaliwa kwa CCM mwaka 1977 katika Uwanja wa Amaan Zanzibar.
Kabla ya kuzaliwa kwa CCM, Jumbe alikuwa Rais wa Chama cha ASP ambapo ushawishi wake mkubwa ndiyo uliosababisha kuunganishwa kwa vyama hivyo na kuzaliwa kwa CCM, ikiwa ni moja ya juhudi za kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika kuimarisha demokrasia na sauti za wananchi kusikika, Jumbe alianzisha chombo cha kutunga sheria ambacho alikiita Baraza la Wawakilishi. Baraza la Wawakilishi liliasisiwa katika mwaka 1979 kwa kuanzia viongozi kutoka katika Wilaya za Unguja na Pemba kwa kuzishirikisha jumuiya za chama ikiwemo Umoja wa Vijana, Wazazi, Ushirika na Umoja wa Wanawake (UWT).
Huo ndiyo mchango mkubwa wa Jumbe katika kuanzisha chombo cha Baraza la Wawakilishi ambalo aliliita ngome ya wananchi katika kusikiliza maoni yao.
CCM yasikitishwa
Wakati huo huo, CCM Zanzibar imeeleza kusikitishwa na kifo cha Jumbe.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, mchango wa Jumbe katika CCM hautasahaulika.
“Chama Cha Mapinduzi kinatoa masikitiko yake makubwa kutokana na msiba mkubwa wa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake wa kwanza Jumbe. Mchango wake hautasahaulika katika Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
Alisema Jumbe alihakikisha kinazaliwa chama kipya kitakachokuwa na nguvu pamoja na sura ya Muungano kwa ajili ya faida ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alisema tangu kuzaliwa kwa chama hicho, kimeendelea kupata mafanikio makubwa ikiwemo kushinda katika chaguzi zote kuanzia za mfumo wa chama kimoja hadi vyama vingi.
Aidha chama hicho kimeendelea kuwa imara bila ya kuyumba na kuendelea kushika hatamu ya kuongoza dola katika kipindi chote kuanzia mwaka 1977 hadi leo.
“Mafanikio yote ya Chama Cha Mapinduzi hatuna budi kukumbuka juhudi zilizofanywa na hayati Jumbe kwa sababu ndiye aliyekiunganisha chama hicho kutoka ASP na TANU na kuzaliwa CCM,” alisema Vuai.
No comments:
Post a Comment