Sunday 14 August 2016

MREMA:MATEJA WASITUPWE JELA

Image result for
MWENYEKITI wa Bodi ya Taifa ya Parole, Augustine Mrema ameshauri waathirika wa dawa za kulevya kupelekwa hospitalini kupata tiba badala ya polisi kuwakamata na kuwapeleka mahabusu au gerezani ambapo huko hujazana bila kupata msaada wowote.
Aidha, amesema atamwomba Rais John Magufuli kumrejesha kazini Mwalimu wa Sekondari, Emmanuel Roman ambaye alifukuzwa kwa ajili ya utumiaji wa dawa hizo, lakini hivi sasa ameacha baada ya kupata tiba na ushauri nasaha.
Mrema alitoa ushauri huo jana Dar es Salaam alipokutana na waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya katika Ukumbi wa Friends Corner, Manzese katika Manispaa ya Kinondoni.
Alisema anapopelekwa gerezani mtumiaji wa dawa za kulevya atakuwa hajasaidiwa, kwani atazidi kuharibikiwa badala ya kurekebishwa.
“Ni marufuku kukamata vijana wadogo wanaotumia kete. Sio kama nahamasisha waendelee kutumia ila wakikamatwa wapelekwe hospitali za Muhimbili, Mwananyamala na Temeke ambako kuna vituo vyao. “Ukianzisha operesheni ya kukamata wezi bila kujua historia zao inawezekana ni waathirika wa dawa za kulevya, ambao wanapoanza kutumia kuacha ni kazi sana hivyo wanalazimika kuiba ili wapate hela ya kununua dawa hizo,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa upande mwingine amevitaka vyombo vya usalama kushughulikia wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo maarufu kama `Mapapa wa dawa za kulevya’, badala ya kuhangaika na hao wanaotumia ili kudhibiti hali hiyo.
“Hili nitalifikisha kwa Rais nimwambie taifa lako linaangamia, vijana wanaharibika kutokana na dawa za kulevya, hivyo awashughulikie mapapa wanaoleta dawa kutoka Iran, kwani wanajulikana kwa majina na wengine wanachukua na kusambaza mtaani,” aliongeza.
Alisema kutokana na janga la dawa za kulevya kuzidi kuwa kubwa nchini, atamwomba fedha Rais Magufuli za kuwasaidia waathirika hao kuunda vikundi vya kuzalisha mali.
Pia ameshauri waathirika hao ambao wameacha watumike kukomesha wizi katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuwakamata mateja ambao wanawajua.
Naye Mwalimu Romani alianza utumiaji wa dawa za kulevya mwaka 1998 akiwa sekondari na aliendelea kutumia hadi alipohitimu kidato cha sita na kwenda chuo cha ualimu, kisha kuanza kazi ambayo aliachishwa kwa kutoonekana kazini kwa muda.
wali, mwathirika wa dawa za kulevya ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kompyuta katika Hospitali ya Mwananyamala, Yusuph Mizito akisoma risala kwa niaba ya wenzake, alisema wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa vituo vya tiba, kwani kwa nchi nzima vipo katika Jiji la Dar es Salaam pekee.


Alisema watumiaji wa dawa hizo ambao wameamua kuacha dawa za kulevya husafiri kupata huduma Dar es Salaam ambako vituo hivyo vipo Mwananyamala, Muhimbili na Temeke.

No comments:

Post a Comment