Monday 15 August 2016

NDUGAI AKUNJUA MAKUCHA

Image result for NDUGAI
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amefunguka na kubainisha wazi kuwa chombo hicho kimekuwa kikifanya kazi zake kwa uhuru bila kuingiliwa na chama chochote cha siasa wala Ikulu kama inavyodhaniwa.
Aidha, amesema kuanzia sasa anaanza kuchukua hatua ikiwemo kuunda kamati ya maridhiano itakayojumuisha maspika wa zamani, kwa ajili ya kujadiliana na pande zote mbili za wabunge kwa maana ya wapinzani na chama tawala ili kutengeneza Bunge lenye maridhiano.
Ndugai, ambaye kipindi kirefu cha Bunge la Bajeti lililomalizika hivi karibuni, alikuwa India kwa matibabu, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza kwenye kipindi cha Funguka kinachorushwa na televisheni ya Azam.
“Nawahakikishia wabunge, mimi nimekuwa kiongozi wa Bunge kwa muda mrefu, nimekuwa na Spika Samuel Sitta na Anne Makinda. Nina zaidi ya miaka 10 ya uongozi katika bunge hili. Sisi katika bunge hatupokei maelekezo kutoka chama tawala (CCM) au Ikulu, tunaendesha bunge kadri tunavyoona na kupitia kanuni tulizonazo,” alisisitiza.
Alisema hisia zilizopo kuhusu dhana hiyo hazina ukweli wowote na zinatokana na dhana ambazo baadhi ya watu wamejijengea kutokana na wanavyoona wao.
Alikiri kuwa hofu na dhana ya chombo hicho kutumika imetokana na uteuzi wa Naibu Spika Dk Tulia Ackson, aliyepewa wadhifa huo, jambo ambalo si la kawaida katika mabunge ya jumuiya madola hali ambayo hata hivyo, haimaanishi kuwa chombo hicho kinatumika.
Alisema bunge hilo limekuwa likitoa nafasi na fursa sawa kwa wabunge wote kuwasilisha hoja zao, ikiwemo kuibana serikali kwa mujibu wa kanuni za bunge na hakuna aliyewahi kunyimwa fursa hiyo.
“Pale bungeni mbunge yeyote ana nafasi kadhaa za kufanyia kazi. Anaweza kuibana serikali kupitia maswali bungeni na nyongeza ya maswali. Ni mbunge gani ambaye ameuliza swali lake halafu sisi bunge tusimpe nafasi, hakuna,” alisema.
Alisema kwa wabunge wanaokosa fursa ya hoja zao kujadiliwa inatokana na hali halisi ya hoja yenyewe huku akitolea mfano wanaowasilisha hoja ya kuahirishwa bunge kwa ajili ya kujadili suala la dharura lililotokea jana au usiku, hali ambayo kiuhalisia haitekelezeki.
Maridhiano ndani ya Bunge
Kuhusu maridhiano ndani ya bunge hilo, Ndugai alikiri kuwa hali ya sasa ya bunge hairidhishi kutokana na machafuko ya kutoafikiana baina ya kambi ya upinzani (KUB) na wabunge wa chama tawala kiasi cha kusababisha wabunge wa upinzani kususa bunge lote lililopita.
Alisema akiwa Spika wa bunge hilo, suala hilo linamsumbua kichwa na amekuwa akitafuta mbinu mbalimbali za kulishughulikia, ikiwemo kuanzisha kamati maalumu ya maridhiano itakayohusisha maspika wa zamani watakaoshirikiana na spika wa sasa kutafuta suluhu ndani ya chombo hicho.
“Katika Bunge la Katiba kanuni za bunge hilo zilimpa mwenyekiti fursa ya kuunda kamati maalumu si ya kudumu ya maridhiano kama kuna jambo linalohitaji kupatiwa ufumbuzi. Katika bunge la kawaida hakuna kanuni hiyo. Ila mambo yanayotokea kwa sasa bungeni yanahitaji kitu cha aina hiyo,” alisisitiza.
Alisema imefika wakati sasa, bunge hilo liazime uzoefu huo wa bunge la Katiba na kuunda kamati hiyo itakayowakutanisha wabunge wa pande zote mbili zenye utofauti na kuangalia tatizo lililopo na kulitafutia ufumbuzi.
Pamoja na hayo, Spika huyo kwa maoni yake alibainisha wazi kuwa tatizo linaloendelea ndani ya chombo hicho ni wasiwasi na mashaka kwa sababu Naibu Spika anatokana na ubunge wa kuteuliwa.
Upinzani kutoka nje
Kuhusu hoja ya wabunge wa upinzani kutoka nje baada ya kutoafikiana na hoja iliyopo, Ndugai, alisema kitendo hicho kimeanza siku nyingi hali inayotoa fursa kwa wabunge wanaobaki bungeni, kupata fursa ya kuwashambulia wabunge wenzao waliotoka.
Hata hivyo, aliwashauri wabunge hao wa upinzani wakiwa kama binadamu lazima wabadilishe mbinu kadri muda unavyozidi kwenda kwani mbinu ya wapinzani hao ya kutoka nje kwa sasa imepitwa na wakati.
Alisema pamoja na kwamba suala hilo ni demokrasia ila wabunge hao wanazo fursa wanazoweza kuzitumia na kufikisha vyema ujumbe wao, hivyo kuendelea kuchangia ndani ya chombo hicho wakiwa kama wawakilishi wa wananchi waliowachagua.
Alitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na kuwasilisha maoni yao kupitia msemaji mkuu wa siku hiyo kutokana na wizara au jambo lililopo mezani au kuchangia katika mijadala iliyopo kwa kuwa wabunge wote wakiwemo wa upinzani na wa chama tawala wamepewa muda sawa kwa uwiano katika kuchangia ndani ya bunge hilo.
“Hakuna hoja ambayo kambi ya upinzani hawana fursa ya kuizungumza, tena huwa wanapanga watu wanaotaka kuzungumza wao wenyewe lakini fursa zote hizo mnaziacha mnatoka nje na kusababisha mazingira ya mle ndani kuchafuka na bunge kuonekana la ajabu,” alisema.
Mikutano ya hadhara na maandamano
Kuhusu hoja hiyo, kiongozi huyo wa bunge, alisema vyama vya upinzani vinayo nafasi kubwa ya kuendeleza siasa zao ndani ya bunge kuliko mitaani kwa kuwa tayari muda wa uchaguzi umepita na sasa ni wakati wa maendeleo.
“Angalieni leo Marekani, Donald Trump na Hillary Clinton leo wanaitana majina ya kila aina, lakini uchaguzi ukiisha hutawasikia, wote wanaungana kuijenga nchi yao, siasa zinabaki ndani ya bunge. Upinzani wana fursa nzuri ya kulitumia bunge, Mkuu wa kambi ya Upinzani anaweza kusimama bungeni wakati wowote na kuwasilisha hoja zake, sioni sababu ya mikutano hii,” alisisitiza.
Adhabu kwa wabunge Akizungumzia suala la baadhi ya wabunge kutoka upinzani kuadhibiwa kutokana na kauli zao ndani ya bunge, Ndugai alisema kila mbunge aliyeadhibiwa, ilitokana na alichokifanya mwenyewe ndani ya ukumbi wa bunge kwa uwazi bila kificho.
Alisema kabla ya adhabu hiyo wabunge wengi waliitwa, kuonywa na kuelekezwa wajirekebishe lakini hawakurekebishika. “Naweza kusema wengi wamejitakia kwa kweli.”
Alisema ndani ya bunge hilo kwa sasa imekuwa ni tatizo kubwa wabunge kutoa kauli au tuhuma dhidi ya viongozi wa serikali bila kuwa na ushahidi na pindi wanapotakiwa kufuta au kuthibitisha kauli zao kwa mujibu wa kanuni za Bunge huwa wanakataa.
“Wanapoambiwa wafute au wathibitishe au tuhuma hizo wanakataa. Inabidi suala lipelekwe kwenye kamati ya maadili ambako kutokana na ukosefu wa ushahidi inabidi waadhibiwe,” alisema.
Alisema mambo kama hayo mengi yangeweza kuepushwa kirahisi kwa mbunge kufuta kauli yake, kuthibitisha au kurekebisha lugha. “Lakini mtu bado anaendelea kusimamia msimamo wake mpaka mwisho.”
Alitoa mfano wa mmoja wa wabunge aliyewahi kutamka ndani ya bunge kuwa Waziri wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), Dk Hussein Mwinyi, aliingia mikataba fulani binafsi na kujengewa nyumba binafsi na jeshi. Waziri huyo alimuandikia spika barua na kulalamika kuwa ametuhumiwa vibaya.
Alisema baada ya malalamiko hayo, bunge likamtaka mbunge aliyerusha tuhuma hizo afute kauli yake au athibitishe tuhuma alizozitoa, lakini alikataa na suala hilo kupelekwa kwenye kamati ya maadili ambako nako hakuwa na ushahidi wowote dhidi ya tuhuma hizo.
“Sasa mtu kama huyu ataacha kupewa adhabu. Yupo mwingine alisema serikali imeleta magari ya washawasha zaidi ya 700, nikamhoji zaidi ya mara tatu kuhusu hoja yake hiyo? Alisisitiza ana uhakika na ushahidi anao ambao alidai ameupata kwenye Jamii Forum naye aliadhibiwa kwa kukosa ushahidi,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa Kanuni za Bunge wabunge wana fursa nzuri ya kujitetea hata pale wanapotoa tuhuma wasio na ushahidi nazo ambapo wanaweza kufuta kwanza kauli zao na kuomba muda wa kutafuta ushahidi ndipo wazitoe kwa uhakika.
Vijembe, kejeli bungeni
Spika Ndugai alikiri kuwa suala la wabunge bila kujali itikadi zao kurushiana vijembe, kutukanana na kukejeliana ndani ya chombo hicho, si jambo zuri na linalitia doa bunge hilo.
Alisema haipendezi hata siku moja kila wakati watu kuondoka kwenye mada iliyopo na kuanza kurushiana vijembe na kutumia lugha za ajabu, hali inayoongeza chuki na kujenga mazingira ya uhasama ambayo hayapendezi. Ndugai alisema watanzania wanaofuatilia chombo hicho wanapata tabu kuona bunge la aina hiyo.
“Nawaomba wabunge kuanzia sasa tutakaporudi Dodoma tubadilike, tupendane, tuheshimiane na kuvumiliana. Matusi, kejeli, vijembe, kanuni zetu haziruhusu lakini hata kiuhusiano haipendezi hata kidogo”.
Aidha aliahidi kuzungumzia suala hilo, katika mkutano wa wabunge wa CCM unaotarajiwa kufanyika siku chache zijazo mjini Dodoma.
Alisisitiza kuwa viongozi wa bunge hilo, wamewavumilia wabunge wote vya kutosha kwa takribani miezi minane iliyopita tangu bunge hilo lianze kazi, lakini kuanzia sasa, hakuna mbunge yeyote atakayeenda nje ya mstari atakayevumiliwa.
Alikiri kuwa mwanzoni viongozi wa bunge walivumilia kwa kuwa takribani asilimia 70 ya wabunge walikuwa ni wapya na hawazifahamu vyema kanuni za bunge ila kwa hatua iliyofikiwa uongozi huo utawachukulia hatua wabunge wote watakaovunja kanuni za bunge.
Utoro wa wabunge
Ndugai alikiri kuwa utoro ni tatizo kubwa linaloendelea kulisumbua bunge hilo, kwani wabunge wengi wamekuwa hawahudhurii vikao vya bunge na wengine pamoja na kuonekana ndani ya ukumbi hutoka kabla ya muda wa vikao kuisha na kuendelea na shughuli zao.
“Natambua hili si tatizo la Tanzania pekee, mabunge mengi ya jumuiya madola, likiwemo la Kenya na Uganda wanakabiliana na tatizo hili. Na hii inatokana na tatizo la kanuni zinazosema kuwa mbunge asipohudhuria mfululizo wa mikutano mitatu anakosa sifa ya ubunge,” alisema.
Hata hivyo, mikutano ya bunge inajumuisha vikao vingi na kusisitiza kuwa kanuni hiyo haina nguvu kwani wengi huweza kuhudhuria kikao kimoja katika mkutano mmoja na kukosa sifa ya kuvuliwa ubunge.
“Tunaangalia namna ya kuishughulikia kanuni hii,” Bunge live Akijibu hoja ya bunge hilo kurushwa moja kwa moja kupitia kwenye runinga, kiongozi huyo wa bunge, alikiri kuwa kwa sasa hakuna uamuzi mwingine zaidi wa huo wa kuzuia matukio ya bunge hilo, kurushwa moja kwa moja hewani.
Alisema labda kama suala hilo litabadilishwa hapo baadaye lakini kwa sasa limeonesha mafanikio kwani sasa mijadala ya wabunge, imekuwa ikifanyika kwa tija kuliko awali ambako wabunge wengi walikuwa wakijadili hoja kwa ‘usanii’ baada ya kuona kamera.
Lugumi
Akijibu hoja kuhusu kashfa ya mkataba tata wa kampuni ya Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi, alisema bado suala hilo lipo mikononi mwa bunge na taarifa yake rasmi inatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano wa bunge wa Septemba au Novemba kwa ajili ya kujadiliwa.
Alisema baada ya kamati ndogo ya bunge kupita nchi nzima na kukuta baadhi ya maeneo vifaa vile vimepelekwa lakini havijafungwa iliamuliwa itengenezwe timu ya ukaguzi mdogo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo itawasilisha taarifa yake bungeni.
“Lugumi bado iko kwetu chini ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC), katika eneo la kuwasilisha taarifa za kamati, PAC itawasilisha taarifa ya kazi zake na Lugumi itawasilishwa kama hoja yenyewe na kujadiliwa,” alisema.
Kuhamia Dodoma
Aidha, Spika Ndugai ameendelea kusisitiza kuwa ofisi yake pamoja na kwamba ilishahamia Dodoma, baada ya misisitizo wa Dk Magufuli aliotuoa hivi karibuni kuhusu serikali kuhamia mkoani humo, asilimia 99 ya shughuli za bunge zitafanyika Dodoma

No comments:

Post a Comment