Thursday, 11 August 2016
JPM:NATAKA KUTENGENEZA TANZANIA MPYA
RAIS John Magufuli amewaambia wananchi wa Sengerema mkoani Mwanza na Watanzania kwa ujumla kuwa wana deni kubwa kwake baada ya kumchagua kwa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, lakini akawaahidi kuwa hatawaangusha na anataka kutengeneza Tanzania mpya.
“Nataka niwaeleze deni limebaki kwetu, nyie mmemaliza kazi yenu. Deni ni ahadi nataka niwaahidi kama nilivyokuja kuwaomba kura sitawaangusha, nataka kutengeneza Tanzania mpya,” alisisitiza Rais Magufuli huku akiwataka wananchi kuendelea kuiamini serikali yake, kwa kuwa iko pamoja nao.
Aidha, Rais Magufuli alisisitiza suala la watendaji wa serikali, kuacha kuwanyanyasa wananchi wanyonge, na badala yake wahangaike na mafisadi na wafanyabiashara wakubwa wanaokwepa kodi, badala ya kuwatoza ushuru wanyonge.
“Kusanyeni kodi kwa wafanyabiashara wakubwa na sio kwa wananchi wanyonge,” alisema Rais Magufuli na kupiga marufuku kwa halmashauri kuwatoza ushuru wakulima wanaosafirisha mazao yao kutoka shambani, na badala yake aliwataka wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote nchini kutoza ushuru huo kwa wafanyabiashara wakubwa wanaosafirisha mazao kwa magari makubwa aina ya Fuso.
“Madiwani mlichaguliwa na wananchi kama nilivyochaguliwa mimi, kama kuna by laws (sheria ndogo) ya kukusanya ushuru wa gunia mbili hadi tatu mkaifute sheria hiyo,” alisema.
Aliongeza kuwa wananchi wanatumia muda na nguvu nyingi katika kulima mazao yao, halafu wanatoka shambani wanakuta mtu anawasubiri akiwa na risiti za ushuru, ambapo aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kulichukulia suala hilo kwa umuhimu wa kipekee.
“Tafuteni kodi kwa watu wenye biashara kubwa na sio wananchi wanyonge, maana watu wakubwa walikuwa hawalipi kodi, na sasa wafanyabiashara wakubwa walipe kodi na wanyonge wastarehe,” alisema na kuongeza kuwa serikali yake inapenda kukusanya kodi, lakini sio kodi inayokusanywa kwa wananchi wanyonge hasa wakulima.
Aidha, alisisitiza kuwa serikali yake haitatoa chakula cha bure kwa Watanzania ambao hawafanyi kazi wakiwa na mawazo ya kusubiri msaada wa chakula kutoka serikalini.
Akiwahutubia maelfu ya wakazi wa Sengerema kwenye Viwanja vya Mnadani wakati wa ziara yake ya siku mbili ya kikazi mkoani Mwanza, Rais Magufuli alisema, “Serikali yangu haina chakula cha bure kwa mtu ambaye hafanyi kazi.”
Aliwashukuru kwa kuwachagua wabunge wazuri wa CCM, William Ngeleja (Sengerema) na Dk Charles Tizeba (Buchosa) ambao alikiri kuwa wote ni wazuri na walishiriki kikamilifu katika kupitisha Bajeti ya Serikali kutenga kiasi cha Sh bilioni 2.5 kwa ajili ya Mahakama ya Mafisadi nchini.
Alisema kuna wakati ilimuwia vigumu wakati anataka kumteua Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, kwa kukiri Dk Tizeba na Ngeleja wote walikuwa na vigezo sawa.
Aidha, alisema serikali itatafuta fedha za ujenzi wa barabara ya Sengerema- Kamanga kwa kiwango cha lami ambayo kwa sasa inafanyiwa upembuzi yakinifu, huku akiwaahidi wananchi wa Busisi kuwa serikali imetenga fedha za ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi, ambalo alisema litafanana na daraja lililojengwa Kigamboni, Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment