KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm amewafungia kazi wachezaji
Haruna Niyonzima na Malimi Busungu kwa kuwapa mazoezi maalumu kwa ajili
ya kuwakabili MO Bejaia ya Algeria.
Yanga itacheza na MO Bejaia mwishoni mwa wiki hii kwenye Uwanja wa
Taifa Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa kundi A wa Kombe la Shirikisho
Afrika huku wenyeji wakisaka ushindi wa kwanza baada ya kupoteza mechi
tatu na kutoka sare mchezo mmoja.
Katika mazoezi ya jana asubuhi, kocha Pluijm alionekana akiwazidishia
dozi wachezaji hao wawili kwa kuwapa mazoezi magumu huku wachezaji
wengine wakifundishwa na kocha msaidizi Juma Mwambusi.
Baada ya mazoezi hayo kumalizika, kocha Pluijm aliliambia gazeti hili
kuwa ameamua kuwaandaa wachezaji hao kwa sababu walikuwa majeruhi kwa
muda mrefu na sasa wamerudi ndiyo maana anawaandaa kwa ajili ya mechi
zinazokuja, ikiwemo ile ya Jumamosi dhidi ya MO Bejaia.
Mshambuliaji Donald Ngoma ataukosa mchezo huo wa Jumamosi kutokana na
kuwa na kadi mbili za njano na nafasi yake inaweza kuchukuliwa na
Busungu na Niyonzima anatarajiwa kuanza kwenye eneo la kiungo baada ya
mchezo uliopita dhidi ya Medeama ya Ghana kuanzia benchi.
Katika hatua nyingine, kocha huyo alisema maandalizi yao yanakwenda vizuri na wachezaji wake wote wapo katika hali nzuri.
No comments:
Post a Comment