Saturday, 13 August 2016

MAGUFULI:NAREJESHA CCM YA NYERERE

Image result for MAGUFULI CCM DAR
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais John Magufuli amesema anataka kuona CCM mpya na kwamba anataka kukirudisha chama katika maadili kama kilivyoachwa na Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Amaan Karume.
Aidha, amewataka wanachama wa chama hicho kumvumilia wakati atakapokuwa akifanya kazi ya kukirudisha kwenye maadili, kwani katika kuifanya kazi hiyo mahali atakapoamua kunyoosha, atanyooshea hapo hapo hata kama kuna kigogo ataondoka.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na wanaCCM pamoja na wananchi waliojitokeza kumshuhudia wakati akiingia katika Ofisi Ndogo za CCM Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kushika wadhifa huo wa uenyekiti Julai 23, mwaka huu, mjini Dodoma.
“Chama Cha Mapinduzi tumepanga tuanze kujisahihisha, kwa sababu chama ninachokipenda nimekulia humu, kilikuwa kimeanza kupoteza dira na hili lazima niliseme wazi bila unafiki,” alisema Rais Magufuli aliyefika katika ofisi hizo saa 5.01 asubuhi akitokea moja kwa moja Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ambako alitua akitokea Mwanza.
Baada ya kuchaguliwa Dodoma, alikwenda ziarani Singida, Tabora, Shinyanga na Geita na kumalizia Mwanza.
Alisema CCM ilikuwa imeanza kugeuka kuwa chama cha matajiri, kwani ilifika mahali kama mtu ni masikini akiomba uongozi ilikuwa ni vigumu kuupata kama vile mtu kupita kwenye tundu la sindano na hilo alijionea mwenyewe.
Akifafanua kuhusu jambo la watu kununua uongozi, mwenyekiti huyo alisema kamwe hatakubali watu watakaotaka kupata uongozi kwa kutumia fedha zao na kwamba anataka sifa za uongozi bila kujali dini, ukabili wala jinsia, bali wenye uwezo wa kuongoza wapewe nafasi.
Alisisitiza mwaka ujao chama hicho kitafanya uchaguzi wa nafasi mbalimbali, hivyo yeyote mwenye uwezo wa kuongoza aombe nafasi na atakayeomba na kutaka kutumia rushwa, atambue kuwa jina lake halitarudi, kwani hata yeye amechaguliwa bila kutumia hata senti.
Alisema anataka mambo yawe mazuri na ndio maana anataka kutafuta mafisadi ndani ya chama hicho, kwani anatambua kuwa wapo na wengine walikimbia mapema huku akiainisha kuwa waliopo atahakikisha analala nao mbele ili kibaki kuwa kipya na chenye maadili kama kilivyoachwa na Mwalimu Nyerere.
“Naitaka CCM mpya chini ya uongozi wangu, ndugu zangu ni lazima tukubali mabadiliko, hata unapotumbua jipu kuna vidamu lazima vitoke,” alisema na kuongeza: “Niko pamoja na ninyi, niko pamoja na chama changu, chama chenye maadili mazuri tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Karume, ninataka kurudisha heshima ya chama hiki,” alisema Dk Magufuli ambaye alichaguliwa kwa asilimia 100 kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Alitoa mfano kuwa chama hicho kina viwanja zaidi ya 400, lakini haijulikani mapato yake yanakusanywa na nani na yanatumikaje, jambo ambalo halisema halikubaliki.
Alisema kuna maghorofa ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), lakini ameambiwa kuna viongozi wamegawana vyumba, alisema hayo ndio atakayoyachambua hadi kieleweke.
Aliendelea kusema ni lazima wanachama wa CCM wahoji kwa nini hata redio ya chama hicho haina matangazo wala fedha, na pia wahoji kwa nini chama kikubwa kama hicho hakina kituo chake cha televisheni. Aliongeza chama hicho kwa sasa lazima kibadilike na kisonge mbele hasa katika suala zima la maendeleo.
Mwenyekiti huyo wa tano tangu kuzaliwa kwa CCM mwaka 1977 aliongeza kuwa Umoja wa Wanawake (UWT) walikuwa na jengo kubwa Morocco na vitega uchumi vingi, Umoja wa Wazazi nao wana vitega uchumi, lakini ni lazima watu wajiulize kuwa mapato yake yanakwenda wapi.
Alisema kuingia kwake ndani ya chama hicho wapo watu ambao hawatafurahi, lakini anaamini wengi watafurahi. Alisema haiwezekani chama hicho kila ikikaribia uchaguzi wanakwenda kuomba kwa wafanyabiashara.
“Haiwezekani UWT nao wakaombe vivyo hivyo, na hata inawezekana waliohama CCM wanafuata, wanavaa mabaibui usiku wanakuwa Chadema, mchana ni CCM… nataka chama kiendelee kutawala milele,” alisema na kutaka wajihoji kuwa kwa nini taasisi za chama hicho hazina fedha. Aliwataka kukubali mabadiliko.
Aidha, Rais Magufuli alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais na Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete kwa kuwa alisimama imara kwa ajili ya kukilinda chama hicho na alisimamia haki, upendo na heshima ya CCM.
Aliahidi kuwa ataendelea kuchota busara za Kikwete pamoja na wenyeviti wengine waliomtangulia, ambao ni Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi ili kukifanya chama hicho kuendelea kuwa bora.
Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alimshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kumtaka aendelee kuwa katika nafasi hiyo na kumuahidi kuendana na kasi yake kwa lengo la kuwasaidia Watanzania hasa wale wanyonge.
Alisema wanaCCM walihitaji Rais Magufuli apate uenyekiti ili wanayoyaona akiyafanya ndani ya serikali ayafanye pia ndani ya chama hicho. Kinana aliwataka viongozi kuwa madalali wa kuuza nafasi za uongozi, huku akiwataka wanachama wenye sifa kujiandaa kwa ajili ya kugombea mwakani.
Hata hivyo, alitoa tahadhari kwa viongozi wenye makandokando wasijihangaishe kuchukua fomu katika uchaguzi huo wa ndani wa chama utakaofanyika mwakani kwa kuwa majina hayatarudi.
Alisema anaamini kutakuwa na mabadiliko makubwa ndani ya chama hicho na kumuahidi kuwa watahakikisha wanafanya kazi zao kwa uadilifu wa hali ya juu ili kutekeleza Ilani ya chama hicho ya uchaguzi kwa umakini.
Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye naye alipata nafasi ya kuzungumza machache wakati akimkaribisha Rais Ofisi ndogo ya Lumumba.
Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema katika kipindi chote cha ziara ya Rais Magufuli mikoani alikuwa akifuatilia kwa makini maagizo yote aliyoyatoa na kumuahidi kuwa alikuwa akinakili kwa ajili ya kutekeleza maagizo hayo.

No comments:

Post a Comment