Friday, 12 August 2016
SIMBA YAMSTAAFISHA MGOSI
KLABU ya Simba imesema mshambuliaji wake mkongwe Mussa Mgosi amestaafu rasmi soka na sasa atakuwa Meneja wa timu hiyo ya wekundu wa Msimbazi.
Kwa mujibu wa msemaji wa Simba, Haji Manara jana, Mgosi ataagwa rasmi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya URA ya Uganda keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mgosi aliwahi kuzichezea timu kadhaa nchini na nje ya nchi ikiwemo Simba, JKT Ruvu, Mtibwa Sugar na Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Manara alisema pia aliyekuwa Meneja wa timu Abbas Ally atakuwa Mratibu wa timu na Nahodha mpya wa timu hiyo ni Jonas Mkude.
Aidha alisema kuwa kiungo Peter Mwalyanzi aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka Mbeya City ametolewa kwa mkopo African Lyon iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.
“Kulingana na usajili uliofanyika msimu huu, timu sasa itakuwa na viungo wengi na ushindani wa namba utakuwa mkubwa, hivyo tumeona Mwalyanzi tumpeleke African Lyon kwa mkopo akapate nafasi ya kutunza kipaji chake,” alisema Manara.
Alisema mchezaji huyo kama atafanikiwa kukuza kiwango na mwalimu akajiridhisha, basi atarejeshwa tena.
Katika hatua nyingine, Manara alisema kikosi cha Simba kilitarajiwa kuingia kambini jana Mbweni, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya URA.
URA walitarajiwa kuwasili jana na leo watacheza mechi ya kwanza ya kujipima nguvu dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Huo utakuwa mchezo wa pili wa kimataifa kwa Simba kucheza baada ya Jumatatu ya wiki hii kuifunga AFC Leopards ya Kenya mabao 4-0, katika mchezo wa kuadhimisha miaka 80 ya klabu hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment