Thursday 25 August 2016

NZEGA YABAINI WANAFUNZI HEWA 4,486

WAKATI kazi ya kubaini wanafunzi hewa ikiendelea nchini kote, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, imebaini wanafunzi hewa 4,486 katika shule zake mbalimbali katika Halmashauri ya Mji na ile ya Wilaya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla alisema Halmashauri ya Wilaya ya Nzega ina wanafunzi hewa 2,357 wakati Halmashauri ya Mji ina wanafunzi hewa 2,129.
Ngupulla alisema, walimu waliosababisha kuwapo kwa wanafunzi hewa, watachukuliwa hatua kali za kinidhamu pamoja na kurejesha fedha ya serikali ambazo zilikuwa zikipotea.
Alisema, walimu walioisababishia hasara serikali, wanapaswa kurejesha fedha hizo haraka na akatoa onyo kali kwa walimu wakuu wengine, kutofanya udanganyifu na kuisababishia hasara serikali.
Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dk Thea Ntara, aliwaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri za mkoa wa Tabora, kuhakikisha wanasimamia uhakiki na kuwabaini wale wanaofanya udanganyifu na kuisababishia hasara serikali.
Dk Ntara alisema, takwimu hizo zitaendelea kubadilika siku hadi siku, hivyo wakurugenzi wanapaswa kusimamia na kuchukua hatua za haraka.
Ofisa Elimu Taaluma wa Mkoa, Kassim Mpanda alisema mkoa unapokea ruzuku zaidi ya Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya fidia ya ada na michango mbalimbali iliyofutwa na serikali.

No comments:

Post a Comment