Sunday, 14 August 2016

MAELFU WAOMBA VIWANJA DODOMA

TANGU Rais John Magufuli atangaze uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma, kumekuwa na mwamko mkubwa wa wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini kutaka viwanja na hadi sasa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) imepokea maombi 3,500 ya watu wanaotaka viwanja.
Aidha, wafanyabiashara katika masoko mbalimbali ya Dodoma wamesema hawana mpango wa kupandisha bei ya vyakula hata serikali itakapohamia rasmi, kwani vipo vingi na wamejipanga kuongeza mitaji ili kuendana na kasi ya ongezeko la watu.
Katika mahojiano na gazeti hili juzi, Ofisa Uhusiano wa CDA, Angela Msimbira alisema mpaka sasa maombi yaliyopokelewa ni takribani 3,500 kwa ajili ya viwanja vya makazi na taasisi mbalimbali.
Alisema wizara karibu zote zimeshatuma maombi ya kupatiwa maeneo, mifuko ya hifadhi ya jamii, makanisa, shule, vyuo, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na watu binafsi.
“Wengi wanaoomba viwanja wanatoka maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam na wamo pia watumishi wa serikali,” alisema Msimbira na kuongeza kuwa, wananchi na wakazi wa Dodoma nao wamehamasika kulipia viwanja. “Kuna watu walipatiwa viwanja na mamlaka tangu mwaka 2009 walikuwa kama wamevitelekeza, lakini sasa wanakuja kuvilipia,” alisema.
Alisema kwa sasa mapato ya mamlaka yanaongezeka kwa kuwa hata wasio na mazoea ya kulipia viwanja sasa wanavilipia.
“Mwamko umeongezeka kwa asilimia 100, kwa siku moja tunapokea wateja hadi 150 ambao wanafika kwenye mamlaka kwa ajili ya kulipia viwanja na kuchukua ‘bili’ (ankara) zao,” alisema Msimbira.
Pia alisema watu wengi sasa wanaulizia kama watapata nafasi ya kupanga katika nyumba za mamlaka wakiwemo watumishi wa serikali na watu binafsi.
Alisema mamlaka ina nyumba 583 zikiwemo 174 za ghorofa ambazo wapangaji wake waliondolewa kwa ajili ya kupisha ukarabati mkubwa unaotarajiwa kufanyika kuboresha nyumba hizo pamoja na mifumo yake. Hata hivyo, alisema baada ya ukarabati kumalizika watapangishwa watu watakaokidhi vigezo vitakavyotolewa na mamlaka.
Pamoja na hayo amewataka wananchi kote nchini wanaohitaji viwanja Dodoma kuvuta subira, kwani utaratibu wa kusanifu viwanja na kuvipima katika maeneo mbalimbali unaendelea. Amesisitiza wasinunue maeneo yasiyopimwa na CDA.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wamesema hakuna hofu ya upatikanaji wa vyakula mjini Dodoma na wala hawana mpango wa kupandisha bei. Mmoja wa wafanyabiashara katika Soko Kuu la Majengo, Ramadhani Muzazi maarufu kwa jina la Langolango alisema mboga na matunda ni mengi na hakuna hofu ya watakaohamia Dodoma kuwa na hofu ya upatikanaji wa vyakula.
“Vyakula viko vingi waje tu, kwani Soko Kuu la Majengo lina wafanyabiashara wengi na limekuwa likihudumia watu wengi hasa wakati wa mikutano inayofanyika mkoani Dodoma ikiwemo mikubwa na hata wakati wa vikao vya Bunge na hawakuwahi kupandisha bei,” alisema Muzazi.
Muzazi ambaye pia ni Mweka Hazina wa Soko hilo, alisema wamefurahi ujio wa makao makuu kwani ni fursa nzuri kwao kufanya biashara na wataboresha huduma ili kuongeza utoaji wa huduma huku Mwenyekiti wao, Godson Rugazama akiwataka kutokupandisha bei ya bidhaa na badala yake waboreshe zaidi huduma zao kwani watakuwa na soko la uhakika wa bidhaa zao.
Mwenyekiti wa Soko la Matunda na Mboga la Sabasaba, Athumani Makole alisema wamefurahishwa na ujio wa makao makuu Dodoma, kwani itakuwa fursa kwao kujiongezea vipato.
Mkazi wa Dodoma, Pudenciana Alfayo alisema kuna haja ya kubadilisha miundombinu ya Soko la Majengo na masoko mengine ili yawe na hadhi ya makao makuu, akitolea mfano Soko la Majengo ni la muda mrefu ili litoe fursa kwa wafanyabiashara kufanya kazi zao katika mazingira mazuri.
“Kumekuwa na kuchakaa kwa miundombinu kama paa la soko, mifereji ya maji taka serikali iangalie namna soko hilo litakavyoboreshwa. Dodoma inaelekea kuwa makao makuu ya nchi Soko la Majengo liboreshwe, ni soko kubwa hapa Dodoma,” alisema Alfayo.
Akizungumzia uamuzi wa kuhamia Dodoma sasa, Waziri wa zamani wa Mawasiliano na Uchukuzi, William Kusila alisema visingizio vya gharama vilikuwa vikikwamisha serikali kuhamia, lakini utashi wa Dk Magufuli utafanikisha hilo kutokana na nia ya dhati aliyokuwa nayo katika kutumikia Watanzania bila kujali hali zao za maisha.
Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili, alisema uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma ni mzuri. Alisema tangu uamuzi huo kutangazwa mwaka 1973 kulikuwa hakuna utashi wa viongozi kuhamia Dodoma huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni gharama.
“Utekelezaji wa uamuzi huo haukuwa na utashi wa serikali kuhamia Dodoma kwani viongozi wengi walipenda kuishi Dar es Salaam,” alisema Kusilla aliyewahi kuwa Mbunge wa Bahi mkoani Dodoma na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo.

No comments:

Post a Comment