Saturday 13 August 2016

MCHUNGAJI MORAVIAN JELA MIAKA 20 KWA MENO YA TEMBO

Image result for MENO YA TEMBO
MAHAKAMA ya Mkoa wa Katavi imemhukumu Mchungaji wa Kanisa la Moravian kijijini Usevya wilayani Mlele, Godwel Siame, kifungo cha miaka 20 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la uhujumu uchumi la kukutwa na meno ya tembo ya uzito wa kilo 20 yenye thamani ya Sh milioni 90.
Hakimu wa Mahakama hiyo, Chiganga Tengwa akisoma hukumu hiyo jana alisema ameridhishwa na ushahidi usiotia shaka yoyote uliotolewa na upande wa mashitaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
“Nimelazimika kutoa adhabu kali ili iwe fundisho sio kwa mshtakiwa tu, bali kwa wengine wenye tabia kama yake,” alisisitiza.
Kwa upande wa mashtaka uliita mashahidi sita huku upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili wa Kujitegemea, Patrick Mwakyusa uliita mashahidi wanne mahakamani hapo.
Awali, Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali Mfawidhi, Achiles Mulisa alieleza mahakamani hapo kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 5, mwaka huu.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa alikutwa na nyara hizo za serikali zenye uzito wa kilo 20 zikiwa na thamani ya Sh milioni 90 zikiwa zimefichwa katika ofisi ya mshtakiwa katika Kanisa la Moravian kijijini Usevya.

Akijitetea, mshtakiwa aliomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwamba lilikuwa kosa lake la kwanza huku akisisitiza kuwa alikuwa hafahamu nyara hizo za serikali zilifikishwaje ofisini kwake kwenye kanisa hilo.

No comments:

Post a Comment