Wednesday, 17 August 2016

UTAFITI:KEMIKALI HIZI ZIKISHIKA MOTO HAZIZIMWI NA MAJI

Vitu vikishika moto, kwa kawaida tunazima moto kwa kuvimwagilia maji. Lakini kemikali zifuatazo zikishika moto, ukizimwagia maji zinaweza kulipuka.
1. Metali za akali
Metali za akali ni pamoja na Lithium, Sodium, Potassium, Rubidium, Cesium na Francium. Metali hizi haziwezi kudumu hewani, zitaungana na hewa ya Oxygen. Ukiziweka majini, zitatoa hewa ya Hydrogen na joto kubwa, joto hili linaweza kutia moto Hydrogen na kusababisha mlipuko.
2. Calcium Carbide
Calcium Carbide ni kemikali muhimu inayotumiwa kuzalisha hewa ya Acetylene viwandani. Kemikali hiyo yenyewe haiwezi kushika moto, lakini ikikutana na maji itabadilika kwa kasi na kutoa Acetylene na joto kubwa. Ni rahisi kwa Acetylene kushika moto.
3. Triethylaluminum
Triethylaluminum ni majimaji maangavu, ambayo yanatumiwa kuzalisha kemikali nyingine au kutumiwa kuwa nishati ya roketi. Inaweza kushika moto yenyewe hewani, ikikutana na maji itatoa hewa ya Ethane na joto kubwa, na mwishowe kulipuka.
4. Majimaji mepesi kuliko maji yanayoweza kushika moto
Petroli, dizeli, Benzene na mafuta ya kupika ni mepesi kuliko maji, tena hayaungani na maji. Majimaji hayo yakishika moto, kumwaga maji hakusaidii kuzima moto, bali kutasababisha majimaji hayo kuenea. Mafuta yakishika moto unapopika, unaweza kuzima moto kwa kuufunika kwa kifuniko cha kikaango.
Kwa ujumla, kemikali zikishika moto, ni lazima uwaarifu wazima moto aina za kemikali ili wachukue hatua maalum ya kuzima moto.

No comments:

Post a Comment