RAIS John Magufuli ametembelea msikiti na makanisa yaliyopo Chato
mjini mkoani Geita na kuendelea kuwasihi Watanzania kuombea amani na
utulivu katika nchi, bila kujali tofauti za dini, makabila na kanda
wanazotoka.
Rais alitoa ujumbe huo mara baada ya kusali ibada ya Jumapili katika
Kanisa Katoliki la Bikira Maria Parokia ya Chato. Baadaye alitembelea
Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Stephano Parokia ya Chato, Kanisa la
African Inland Church la Chato na kumalizia katika Msikiti wa Omar
Bin-L-Khattab wa Chato.
Rais Magufuli alisema pamoja na Watanzania wote kuungana kuombea
amani na utulivu, pia hawana budi kutekeleza kwa vitendo maandiko
matakatifu ya Biblia yasemayo “Asiyefanya kazi na asile” kwa kuhakikisha
kila mmoja anachapa kazi kwa juhudi na maarifa ili kuharakisha
maendeleo ya Taifa.
“Ndugu zangu nawashukuru sana, muendelee kuliombea taifa hili, taifa
letu ni la umoja, sisi wote ni Watanzania, tuendelee kumuomba Mola wetu,
kudumisha amani yetu, kujenga umoja wetu kwa dini zote, makabila yote
na vyama vyote, kwa sababu Mola wetu anatupenda sisi sote,” alisema Rais
Magufuli.
Aidha, baada ya kuwasalimu waumini wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria
Parokia ya Chato, Rais Magufuli aliendesha harambee ya kuchangia ujenzi
wa jengo jipya la kanisa hilo, ambapo Sh milioni moja zilikusanywa papo
kwa hapo.
Tayari Rais Magufuli alishachangia ujenzi huo kwa kutoa Sh milioni moja Aprili 3, mwaka huu.
Alitoa wito kwa watu mbalimbali, kujitokeza kuchangia ujenzi wa
kanisa hilo. Katika Msikiti wa Omar Bin-L-Khattab na makanisa ya
Anglikana na African Inland, Rais Magufuli alichangia Sh milioni tano
kwa kila moja kwa ajili kuendeleza na kukarabati majengo.
Kitwanga aandaa Ibada
Katika hatua nyingine, Watanzania wametakiwa kumuombea Rais Magufuli
ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake ya kitaifa na kuleta maendeleo
endelevu nchini.
Pia wametakiwa kumgeukia Mungu kwa kulikubali neno lake, ambalo
limeelezwa ni neno la uzima litakalowakomboa kutoka kwenye utumwa wa
dhambi.
Hayo yameelezwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza,
Askofu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi alipokuwa akitoa mahubiri kwenye ibada
maalumu ya kumuombea Rais Magufuli na familia ya Mbunge wa Misungwi,
Charles Kitwanga (CCM) iliyofanyika nyumbani kwa mbunge huyo.
“Kwenye maisha, Mkristo ukiwa mwangalifu unayo fursa ya kuyaona
maisha ya Mungu na utukufu wake,” alisema na kuongeza; “Niwaombe mbali
na kuikumbuka familia hii ya Mheshimiwa Kitwanga kwa maombi, naomba
tuendelee kumuombea Rais wetu mpendwa John Magufuli ili kusudi yale
aliyoyapanga kuyatekeleza, ayatekeleze kwa ajili ya maendeleo ya nchi
yetu,” alisema.
Alisema Rais kama Mkuu wa nchi, anayo majukumu mazito ya kuongoza
nchi, ambapo alisema ni vyema wananchi kwa umoja wao wakawa wanamkumbuka
kwenye maombi.
Aliwataka wanadamu kumfuata Kristo kwa sababu ni utimilifu wa torati
na utimilifu wa manabii na unabii, ambapo pia alitumia fursa hiyo
kuwataka Watanzania na Wakristo watambue kuwa neno la Mungu, si neno la
udaku wala kuzusha, bali ni injili bora ya Yesu Kristo kwenye maisha
yao.
“Watu wengi tuna utapiamlo wa kiroho kutokana na kutojihusisha na
mambo ya kiroho,” alisema na kuwataka Wakristo nchini na Watanzania wawe
tayari kumpokea Yesu Kristo kwenye maisha yao.
Kwa upande wake, Kitwanga alisema kuwa ameamua kufanya ibada hiyo kwa
lengo la kumuombea Rais Magufuli ili aendelee kutekeleza vyema majukumu
yake kama Rais wa nchi.
Aliwataka wananchi wa Misungwi, watambue kuwa uchaguzi umekwisha na
kwamba kilichobaki kwao ni kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za
maendeleo ili kuijenga Misungwi mpya yenye maendeleo.
Alimshukuru Askofu Ruwa’ichi kwa kuendesha ibada maalumu hiyo, ambayo
imeleta faraja kubwa ndani ya familia yake na wananchi wa Misungwi.
Meya awapasha madiwani
Wakati hayo yakijiri, Watanzania wameombwa kutomchosha Rais Magufuli
kwa kutaka kufanyiwa mambo madogo ya maendeleo, ambayo yako ndani ya
uwezo wao, badala yake wajenge tabia ya kujitoa na kutumia uwezo wao
katika kujiletea maendeleo.
Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Meya wa Ilemela, Renatus
Murunga wakati alipokuwa akijibu madai ya madiwani kwenye kikao cha
Baraza la Madiwani kilichofanyika mjini hapa.
Alisema ipo tabia iliyojengeka miongoni mwa Watanzania na wanasiasa,
kudhani kuwa kila jambo la maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule za msingi
na sekondari, utafanywa na Rais Magufuli.
“Shule za msingi ni zetu wenyewe si za Rais Magufuli, kila mtu,
mtumishi wa umma, kiongozi wa kisiasa ana wajibu wa kuhakikisha mtoto
wake anapata elimu, haiwezekani sasa mwananchi akae akisubiri msaada
kutoka serikalini kwa ajili ya maendeleo yake,” alifafanua.
Alisema kwa upande wa maendeleo, Serikali haina uwezo wa kufanya kila
kitu na kwamba wananchi nao wana mchango wao katika kuiletea nchi
maendeleo, ambapo alimtaka kila Mtanzania awajibike kwenye eneo lake.
“Haiwezekani Serikali ilipe mishahara ya watumishi, ichimbe matundu
ya vyoo, itengeneze madawati, hebu tujenge tabia ya kuwekeza kwenye
shughuli za maendeleo na elimu kwa ajili ya watoto wetu,” aliongeza.
Alisema ipo tabia ya baadhi ya watu, kugeuza mambo ambayo yamo ndani
ya uwezo wao na kuyaona kama changamoto kwao, wakisubiri msaada kutoka
Serikali Kuu wakati yanaweza kutatuliwa na wao wenyewe.
“Badala ya kumtegemea Rais Magufuli ambaye ana majukumu ya kitaifa na
kimataifa, mambo mengine tuyafanye sisi wenyewe, hivi kweli hata ujenzi
wa matundu ya vyoo tumsubiri Rais aje atujengee,” alihoji.
Aliwataka madiwani waendelee kuwahamasisha wananchi kwenye maeneo
washiriki kikamilifu kwenye shughuli za uzalishaji mali na maendeleo,
ambapo alisisitiza kuwa suala la maendeleo halina ushabiki wa kisiasa.
No comments:
Post a Comment