Tuesday 9 August 2016

SIMBA YAIONYESHA KAZI AFC LEOPARDS

Image result for simba club VS FC LEOPARDSIMBA jana ilisherehekea vizuri miaka 80 tangu ilipoanzishwa baada ya kuichabanga AFC Leopards ya Kenya mabao 4-0 katika mchezo wa tamasha la `Simba Day’ kwenye Uwanja wa Taifa.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog juzi aliwataka wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa kushuhudia kikosi kitakachotwaa taji la Tanzania Bara msimu wa mwaka 2016/2017.
Simba ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 38 lililowekwa kimiani na Ibrahim Ajibu baada ya kupiga shuti kali la moja kwa moja akipokea pasi ya Mussa Ndusha.
Mchezaji hodari Laudit Mavugo alidhihirisha makali yake pale aliposaidia kupatikana kwa bao la pili lililofungwa tena na Ajib baada ya kumtengenezea mpira safi alioujaza wavuni katika dakika ya 57.
Shiza Kichuya aliyejiunga akitokea Mtibwa, aliiandikia Simba bao la tatu katika dakika ya 66 akimalizia kazi nzuri ya Ajibu na Mavugo, ambao waligongeana vizuri kabla mpira haujamkuta mfungaji aliyeujaza wavuni. Wekundu hao wa Msimbazi waliandika bao la nne lililofungwa na Mavugo baada ya kufanya kazi nzuri uwanjani.
Simba awali walikosa mabao mengi na hii ilitokana na kutoelewana kwa Frederic Blagnon na Kichuya. Wenyeji Simba walifanya shambulizi la nguvu katika dakika ya 28 na kupata kona kupitia kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Hata hivyo, kona hiyo haikuzaa matunda. Awali, Ajibu nusura aigharimu timu yake baada ya kumchezea rafu Jack Kiyai wa AFC Leopards na kupatiwa kadi ya njano katika dakika ya 35 na kuamuriwa upigwe mpira wa adhabu, ambao haukuzaa matunda.
Safu ya kiungo ya Simba imeonekana kuimarika zaidi ikiongozwa na Jonas Mkude, ambapo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu hiyo ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Katika kuadhimisha miaka 80 tangu kuzaliwa kwa klabu hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, Hamisi Kingwangalla, Profesa Athumani Kapuya, Mohamed Dewji `Mo’, pamoja na viongozi wa Simba, walikata keki wakati wa mapumziko.
Simba: Vicent Agban, Jonas Mkude, Mohamed Hussein, Janyie Buifunga, Novaty Lufunga, Method Mwanjale, Mwinyi Kazimoto, Mussa Ndusha, Frederic Blagnen, Ibrahim Ajib na Shiza Kichuya.

No comments:

Post a Comment