KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm amesema Obrey Chirwa ni bonge la
mchezaji ambaye anahitaji mtu mwenye kasi kama yake ili kuendana naye
katika ufungaji magoli.
Pluijm alisema hayo juzi Dar es Salaam baada ya mchezo wa kirafiki
kati ya Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar waliotoka sare ya bila kufungana.
Alisema Chirwa alionesha kiwango bora katika mchezo huo isipokuwa
udhaifu ulionekana hasa baada ya kukosekana kwa mchezaji mwenye mbio
sawa na zake na matokeo yake nafasi nyingi alizokuwa akizitengeneza
mchezaji huyo zilikuwa zikipotea.
Mchezaji huyo aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea FC Plutinum ya
Zimbabwe amekuwa akipangwa katika mechi mbalimbali sambamba na
mshambuliaji Donald Ngoma ambaye hakuwepo katika mchezo wa juzi. Kocha
huyo aliwapumzisha baadhi ya wachezaji tegemeo kwa ajili ya maandalizi
ya mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mo Bejaia.
“Chirwa ni mchezaji mzuri mwenye kasi ambayo akipata mwenzake wa kuendana naye watafanya vizuri,” alisema.
Akizungumzia mchezo huo, alisema Mtibwa Sugar imekuwa ikicheza mchezo wa kujihami zaidi.
Kwa upande wake, Kocha wa Mtibwa Sugar Salum Mayanga alisema
amegundua kikosi chake kina upungufu katika nafasi ya kiungo, hivyo
mchezo huo umemuonesha kasoro anayohitaji kuifanyia kazi.
Yanga inatarajiwa kuingia kambini leo kwa ajili ya maandalizi ya
mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mo Bejaia utakaochezwa
mwishoni mwa wiki hii.
No comments:
Post a Comment