Friday, 12 August 2016
TANZANIA YAPOROMOKA FIFA
TANZANIA imeporomoka kwa nafasi moja katika orodha ya ubora wa viwango vya kimataifa, Fifa iliyotolewa jana na Shirikisho hilo la soka.
Kwa mujibu wa viwango hivyo, Tanzania ipo kwenye nafasi ya 124 kutoka 123 iliyokuwa kwenye viwango vya Julai mwaka huu. Kuporomoka kwa nafasi hiyo moja ni kutokana na timu hiyo kutocheza mechi yoyote ya kimashindano kwa Julai.
Septemba mwaka huu, Timu ya taifa, Taifa Stars inatarajia kucheza mechi ya kimataifa kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa dhidi ya Nigeria, mechi ambayo itakuwa ya kukamilisha ratiba kwani si Stars wala Nigeria yenye nafasi ya kufuzu michuano hiyo itakayofanyika Gabon mwakani.
Algeria imeendelea kuongoza kwa upande wa Afrika ikiwa nafasi ya 32, ikifuatiwa na Ghana ili nafasi ya 35 na Ivory Coast ya 36. Senegal iko nafasi ya 41, Misri ikishika nafasi ya 43, Tunisia ya 45, Morocco ikishika nafasi ya 53 na Cameroon ni ya 54.
Kama ilivyo kawaida kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Uganda bado inashikilia usukani kwa kushika nafasi ya 65 duniani, ikifuatiwa na Kenya nafasi ya 88, Rwanda 121 na Burundi 123.
Nafasi ya 130 imeshikiliwa na Ethiopia, Sudan ya 141, Sudan Kusini 153, Djibouti, Eritrea na Somalia zipo nafasi ya 205.
Argentina imeendelea kukaa kileleni mwa orodha hiyo kama ilivyokuwa mwezi uliopita ikifuatiwa na Ubelgiji, Colombia, Ujerumani, Chile, Ureno, Ufaransa, Hispania, Brazil na Italia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment