BAADHI ya wasomi na wanasiasa wamepongeza hatua ya serikali kutangaza
mwongozo mpya kuwa kuanzia sasa masomo ya sayansi ni lazima kusomwa na
wanafunzi wote, wanaosoma elimu ya sekondari kuanzia Kidato cha Kwanza
hadi cha Nne.
Kwa mujibu wa wadau hao katika elimu, wamebainisha wazi kuwa elimu ya
sekondari kwa maana ya Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Nne, ndio
msingi mkuu wa elimu katika mataifa mengi hivyo inapaswa kupewa
kipaumbele.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu maoni yake kutokana na mwongozo
huo, Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT - Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo,
alisema uamuzi huo wa serikali ni mzuri, lakini kunahitajika jitihada
zaidi za kujenga mazingira mazuri ya kusomea masomo hayo.
Alisema awali wanafunzi hao wa sekondari, walikuwa wakichagua masomo
na wengi kuyaacha masomo ya sayansi kutokana na uhaba wa vifaa vya
sayansi kuanzia Kidato cha Tatu, ambako elimu ya vitendo ni ya lazima
kwa masomo hayo.
“Lakini pia walikuwa wakitakiwa kuchagua masomo ya kuendelea nayo ili
kuwapunguzia wanafunzi idadi ya masomo ya kujifunza ila sababu hii si
ya maana sana, ni vizuri wanafunzi wakasoma masomo yote ya sayansi hadi
Kidato cha Nne kama tulivyofanya sisi,” alisema Profesa Mkumbo.
Alisema sayansi ndio msingi wa elimu ya ufundi, ambayo Chama cha ACT
kimekuwa kikiupigania. “Huu uamuzi ni mzuri lakini mazingira ya kusoma
sayansi yatengenezwe,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema
msingi mkubwa wa nchi yoyote, lazima elimu inayotolewa katika nchi hiyo
ikidhi matakwa na dira ya taifa husika. Alisema uamuzi huo wa serikali
ni muafaka kwa kuwa mwongozo huo, umelenga kukidhi mahitaji ya maendeleo
ya taifa.
“Kimsingi hili wazo linakubalika, hapo mwanzo tulijisahau sana
tulianzisha michepuo mingi mara kilimo, biashara nakadhalika, tukasahau
dira yetu nini. Elimu ya sekondari ndio msingi wa elimu tukijipanga
vizuri hapa, tutatengeneza taifa lenye wasomi wenye tija kwa taifa
letu,” alisisitiza Dk Bana.
Hivi karibuni, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza mwongozo mpya kuwa kuanzia
sasa masomo ya sayansi ni lazima kusomwa na wanafunzi wote, wanaosoma
elimu ya sekondari kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Nne.
Alisema hivi sasa nchi imedhamiria kuingia kwenye uchumi wa kati,
ambao ni wa viwanda, hivyo suala la sayansi haliwezi kuepukwa kwa sababu
ni wakati sasa wa kuwa na wataalamu wengi wa fani za sayansi,
watakaoweza kutosheleza mahitaji ya sekta ya viwanda nchini.
No comments:
Post a Comment