Tuesday, 9 August 2016

AFISA KILIMO ASIMAMISHWA KAZI

Image result for MALINYI MOROGOROMKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, Marcelin Ndimbwa amemsimamisha kazi mara moja Ofisa Kilimo na Umwagiliaji wa wilaya hiyo, Martin Mhode kwa tuhuma ya kukaidi maagizo ya wakuu wake wa kazi.
Pamoja na kudaiwa kukaidi maagizo ya Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Ofisa Kilimo huyo amedaiwa kushindwa kusaidia kufanikisha agizo la Rais John Magufuli la kuwataka watendaji wa serikali kuwasimamia wananchi kufanya kazi.
Akizungumza na gazeti hili mjini Malinyi wakati wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima ya Nanenane, Ndimbwa alisema Ofisa Kilimo huyo alikaidi agizo la kumtaka kuhakikisha matrekta ya halmashauri hiyo, yanapelekwa mashambani muda wote ili kulima mashamba ya wakulima.
“Mimi na Mkuu wa Wilaya tuliagiza matrekta ya halmashauri kuwepo mashambani na kulima muda wote ili kufanikisha malengo ya halmashauri katika kuhamasisha wakulima waliounda vikundi kushiriki katika kilimo cha umwagiliaji ndani ya mradi wa umwagiliaji wa halmashauri. “Lakini kinyume cha maagizo hayo, alikaidi na kuagiza matrekta yatoke shambani na yaegeshwe katika ofisi za Halmashauri kwa kisingizio kwamba amechukua hatua hiyo kutokana na wananchi kugoma kusafisha mashamba,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kitendo hicho ni upuuzwaji wa mamlaka za serikali na pia kinakwamisha maagizo ya Rais ya kutaka viongozi kuwa chachu ya kuwafanya wananchi, kupenda kufanya kazi kwa bidii ili kujiharakishia maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
“Kama mnavyokumbuka hivi karibuni wakati akiwahutubia wakurugenzi, Rais alitutaka kuwasimamia watendaji katika ngazi za halmashauri kuhakikisha mipango ya maendeleo inafanikiwa na si inarudi nyuma. “Ni jambo la ajabu, Ofisa Kilimo anakwamisha jitihada za kukuza kilimo, kwa visingizio visivyo na msingi. Kazi yake ni kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kilimo ili kujiharakishia maendeleo na si kukwamisha mipango tuliyojiwekea,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo amewataka Ofisa Kilimo na Umwagiliaji Msaidizi, Samwel Kuziganita na Ofisa Mifugo, Absalum Gepson kutoa maelezo ya kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kazi, kwa kufanya kazi kwa mazoea na chini ya kiwango ndani ya halmashauri hiyo.

No comments:

Post a Comment