Sunday, 14 August 2016

YANGA MAMBO SAFI

Image result for YANGA
YANGA jana ilipata ushindi wa kwanza kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi baada ya kuishinda bao 1-0 timu ya Mo Beijaia ya Algeria katika mechi ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Matokeo hayo ni kama Yanga imelipa kisasi baada ya timu hiyo kuifunga Yanga bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Algeria. Huo ni ushindi wa kwanza kwa Yanga tangu iingie hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kupoteza mechi tatu na kutoka sare moja.
Jana ilicheza mechi ya tano na hivyo inasubiri kucheza mechi ya mwisho dhidi ya TP Mazembe ugenini Lubumbashi Congo DR mwishoni mwa mwezi huu. Bao la Yanga jana lilifungwa katika dakika ya tatu kupitia kwa mchezaji wake Mrundi Amisi Tambwe.
Tambwe alifunga bao hilo baada ya kuunganisha mpira wa adhabu wa Juma Abdul kabla ya kutokea piga nikupige langoni mwa Bejaia na mpira kujaa wavuni. Katika mechi hiyo ya jana Yanga ilitawala katika vipindi vyote vya mchezo na wachezaji wake Obrey Chirwa na Simon Msuva wakikosa mabao mara kwa mara.
Ushindi huo umefufua matumaini kwa Yanga ambayo ilionekana kuwakatisha tamaa baadhi ya mashabiki wake kwa matokeo mabaya ya awali.
Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa bado wanaendelea kuwa mkiani mwa msimamo wa kundi A wakiwa na pointi nne huku Mazembe ikiongoza kwa kuwa na pointi 10 huku Mo Bejaia na Medeama zikishika nafasi ya pili na ya tatu kwa kuwa na pointi tano kila moja.
Mazembe inacheza na Medeama leo na kama itashinda, Yanga inabidi iombe Medeama na Mo Bejaia zitoke sare na yenyewe (Yanga) iifunge Mazembe katika mechi za mwisho ili iungane na mabingwa hao wa zamani wa Afrika kufuzu hatua ya nusu fainali. Endapo hayo yatatokea Yanga itafikisha pointi saba na kuungana na Mazembe ambayo itakuwa na pointi 13 kwenda nusu fainali.
Yanga: Deogratius Munishi, Deus Kaseke, Mbuyu Twite, Obrey Chirwa, Vincent Bossou, Juma Abdul/ Said Makapu, Thabani Kamusoko, Amis Tambwe, Haji Mwinyi, Simon Msuva na Andrew Vincent/ Kelvin Yondani.

No comments:

Post a Comment